TANZIA: SPIKA MSTAAFU SAMWEL SITTA AFARIKI DUNIA, RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI
Tanzania imepata pigo kubwa baada ya kumpoteza spika mstaafu na mbunge mstaafu wa jimbo la Urambo mkoani Tabora.
Mhe. Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali
ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa
matibabu tangu mwezi uliopita.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli
amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha
Mhe. Samwel Sitta na kwamba Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa
mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa
uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika
kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na
Serikali.
“Kupitia kwako Mhe. Spika naomba
kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na
watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt. Magufuli amesema anaungana na
wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo
wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amen"


Leave a Comment