RUVU SHOOTING: HATUTACHEZA NA YANGA
Uongozi wa timu ya Ruvu Shooting umesema kwamba, timu yao
haiko tayari kucheza mchezo wa ligi kuu kesho dhidi ya Yanga endapo Bodi
ya Ligi/ TFF watashikilia msimamo wao wa mchezo huo kuchezwa kesho
katika uwanja wa Uhuru, Dar es salaam.
Maamuzi hayo yamefikiwa na uongozi wa timu chini ya
Mwenyekiti wake Kanali Charles Mbuge muda mfupi baada ya timu hiyo
kuwasiri Mlandizi saa 4.15 asubuhi ya leo, Novemba 8,2016 ikitokea
Kagera ambapo Jumapili iliyopita, Novemba 6, 2016 ilicheza na Kagera
sugar katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Kanali Mbunge alisema, katika hali
ya uchovu waliyonayo wachezaji baada ya kusafiri safari ndefu ya zaidi
ya KM 1450 kwa basi na kutumia zaidi ya saa 22 kufika mwisho wa safari
ni ajabu kufikia mchezo mwingine wa ligi bila kupumzika japo kwa saa
chache.
Kanali Mbunge alisema, kuwapeleka wachezaji uwanjani kwa
mazingira ya namna hiyo, si tu kuwachosha bali ni kuwasababishia madhara
makubwa kiafya ambayo yanaweza kuwasababishia kifo, kwa hali hiyo
akasisitiza kutoipeleka timu uwanjani kesho kucheza na Yanga katika
uwanja wa Uhuru, Dar es salaam.
Aidha Kanali Mbunge alisema, mbali na madhara ya kiafya kwa
wachezaji, mchezo huo ukichezwa kesho, timu yake haitatoa ushindani
wowote kwa timu pinzani kwani, wachezaji wamechoka sana, miongoni mwao
wakiwa ni majeruhi ambao hawataweza kabisa kucheza mchezo huo kwa siku
ya kesho.
Kanali Mbunge alisema, kuliko kuwaua wachezaji kwa
kuwafanyisha kazi ngumu kama punda bila kupumzika, ni vema tupoteze
pointi kwa kutopeleka timu uwanjani, hao wapinzani wetu wapewe huo
ushindi wa chee.
Awali mchezo huo uliahirishwa kupisha mchezo wa Yanga wa
Kimataifa na kupangwa uchezwe Novemba 10, mchezo huo ulibadilishwa na
kupangwa uchezwe Novemba 11, baadaye ukabadilishwa tena ukapangwa
Novemba 10, hatimaye jana ukabadilishwa na kupangwa uchezwe Novemba 9.


Leave a Comment