OBAMA AMUONYA TRUMP KUWA HATOKAA KIMYA ENDAPO ATAVUNJA MISINGI YA URAIS

 Rais mteule Donald Trump akiwa na Rais anayemalizia madaraka Barrack Obama
Rais wa Marekani anayeondoka Barack Obama amesema huenda akazungumza, kinyume na utamaduni wa siasa Marekani, iwapo mrithi wake Donald Trump atatishia "maadili muhimu" ya Marekani.
Huwa desturi kwamba marais wa zamani wa Marekani huwa hawajiingizi sana katika siasa baada ya kuondoka madarakani na huwa hawazungumzi kuhusu warithi wao.
Akiongea katika kikao na wanahabari wakati wa mkutano wa nchi za Asia na Pasifiki (Apec) mjini Lima, Peru, Bw Obama amesema anakusudia kumsaidia Bw Trump na kumpa muda wa kueleza maono yake.
Lakini amesema kwamba, kama raia, huenda akalazimika kuzungumza kuhusu baadhi ya mambo.
"Ninataka kuiheshimu ofisi na kumpa rais mteule fursa ya kueleza msimamo wake na mipango yake bila mtu kujitokeza kumkosoa," Bw Obama alisema.
Lakini akaongeza, kwamba iwapo suala "litagusa maadili muhimu ya Marekani na imani yetu, na nafikiri kwamba inahitajika au itafaa kwangu kutetea maadili hayo, bado nitalitathmini wakati huo".
Kisha, amejieleza kama "raia wa Marekani anayejali sana taifa"
 
Bw Obama amekihutubia katika kikao na wanahabari mkutano wa Apec mjini Lima, Peru

No comments

SIRI ZA JAMII. Powered by Blogger.