MKE WA RAIS MAGUFULI ARUHUSIWA KUONDOKA MUHIMBILI
Mke wa Rais wa Tanzania John
Magufuli, Janeth, aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya taifa ya
Muhimbili ameruhusiwa kuondoka hospitalini.
Ikulu ilitoa picha ya Rais Magufuli akimjulia hali katika wodi ya Sewa Haji Alhamisi ingawa haikusema alikuwa anaugua wapi.
Taarifa
nyingine iliyotolewa na ikulu Ijumaa imesema ameruhusiwa kuondoka
hospitalini baada ya afya yake kuimarika na akarejea nyumbani.
Ikulu imesema Mama Janeth Magufuli alilazwa hospitalini Jumatano baada ya "kuugua ghafla na kupoteza fahamu".
"Namshukuru
sana Mungu kwamba afya yangu imeimarika, pia napenda kuwashukuru
Madaktari na Wauguzi, nimepata huduma nzuri sana maana siku nilipoletwa
hapa nilikuwa sina fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya lakini
mmenipigania na leo narudi nyumbani nikiwa na afya imara," alisema kabla
ya kuondoka hospitalini.
Naomba pia niwashukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishie
kuwa sasa nipo vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani ambako
nitamalizia matibabu yangu."
Novemba mwaka jana, siku chache baada
ya kuapishwa hospitali hiyo ni miongoni mwa taasisi za serikali ambapo
Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza.
Alisema alisikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini.
Aidha, alikuta baadhi ya vifaa vya kufanyia kazi na mashine muhimu
za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN vikiwa havifanyi kazi
kwa muda wa miezi kadhaa.
Alibadilisha usimamizi wa hospitali hiyo.
Taarifa
ya ikulu ilisema Alhamisi, Rais Magufuli alipofika kumjulia hali mkewe,
wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Sewa Haji walimshukuru "kwa hatua
zilizochukuliwa na serikali kuboresha hospitali ya taifa ya Muhimbili na
wamebainisha kuwa licha ya kuboreshwa kwa mazingira ya hospitali, pia
wanapata huduma nzuri kutoka kwa madaktari na wauguzi."


Leave a Comment