TCU YAONGEZA MUDA WA UDAHILI VYUO VIKUU
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
(TCU) imeongeza muda wa udahili wa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na
vyuo vikuu mwaka wa masomo 2016/2017 ili kuwapa fursa waombaji ambao
wana sifa lakini hawakupata vyuo kutokana na ushindani wa vyuo na kozi
walizozichagua.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu
Mtendaji wa TCU Prof. Eleuther Mwageni alipokuwa akiongea na waandishi
wa habari juu ya mwenendo mzima wa udahili kwa mwaka wa masomo
2016/2017, leo Jijini, Dar es Salaam.
“ Tume imekamilisha awamu ya
kwanza ya udahili kwa waombaji wenye sifa ya kidato cha 6, ambapo jumla
ya waombaji wote ilikuwa 55,347, waombaji wenye sifa ni 47,203 sawa na
asilimia 85.3 ya waombaji wote. Katika waombaji hao wenye sifa waliopata
vyuo ni 30,731 sawa na asilimia 65 na waombaji 16,472 ambao wana sifa
sawa na asilimia 35 hawajapata vyuo hadi sasa, waombaji waliokosa sifa
ni 8,144,” alifafanua Prof. Mwageni.
Amesema kuwa Tume imeamua
kuongeza muda wa udahili kuanzia Septemba 12 mpaka Septemba 23, 2016 ili
kuwapa nafasi waombaji wenye sifa, fursa ya kuomba tena vyuo na kozi
zenye nafasi kutokana na wengi wao kuomba vyuo na kozi za aina moja.
Prof. Mwageni alivitaja vyuo
ambavyo vimeombwa na waombaji wengi na tayari vimeshajaa kuwa ni Chuo
cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha
Afya na Sayansi Shirikishi, Chuo Kikuu cha Kikristo cha Tiba
Kilimanjaro(KCMUCo) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili.
Pia alizitaja kozi ambazo
zimechaguliwa na waombaji wengi kuliko nafasi zilizopo kuwa ni kozi ya
Ualimu, Udaktari wa Binadamu, Ufamasia, Uhandisi, Sayansi ya Uthamini wa
Ardhi na Sheria. Alitoa mfano wa kozi ya Ualimu Chuo Kikuu Kishiriki
cha Ualimu Dar es Salaam ilikuwa na waombaji 15,803 wakati nafasi ni
1,000.
Hivyo amewashauri waombaji
waliokosa nafasi kuomba vyuo na kozi zisizo na ushindani ili waweze
kupata nafasi kwa awamu hii ya pili.
Aidha Tume hiyo imepunguza
viwango vya udahili kwa waombaji wenye sifa ya stashahada kutoka GPA 3.5
mpaka 3.0. Hivyo wamewataka waombaji wenye vigezo hivyo kuomba vyuo na
kwa wale waliomba awamu ya kwanza hawatatakiwa kuomba tena bali kusubiri
matokeo ya waombaji wenye sifa ya stashahada.

Leave a Comment