MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE: FAHAMU MAMBO 11 AMBAYO MWALIMU ALIYAPINGA NA KUKEMEA VIKALI


Image result for mwalimu nyerere
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Mwalimu Nyerere ni Rais wa kwanza na ni muasisi aliyeliletea taifa hili uhuru wa kweli toka katika makucha ya mkoloni 9 December, 1961. Mwalimu Nyerere alizaliwa April 22, 1922 katika kijiji kidogo cha mwitongo huko Butihama, kasikazini mwa Tanzania karibu kabisa na ziwa Victoria . 

Alikuwa ni mototo wa chifu Burito Nyerere wa kabila dogo la wazanaki

Nyerere alifariki dunia kwa ugonjwa wa kansa ya damu, siku ya Alhamisi Oktoba 14, 1999 saa 4:30 asubuhi [kwa saa za Afrika Mashariki], katika hospitali ya Mtakatifu Thomas London, Uingereza akiwa amezungukwa na timu ya madaktari bingwa.

Ndipo wananchi wote tulipigwa na butwaa kwa kumpoteza kiongozi mwenye msimamo thabiti na busara duniani. 
Mwalimu bado ni taa inayong’aa gizani, umuhimu wake nazidi kuonekana kadiri miaka inavyokwenda licha ya kwamba amekwisha tuacha.

Wakati wa uhai wake Mwalimu Nyerere alichukia na kukemea vikali mambo yasiyofaa kwa mustakabali wa maendeleo ya Tanzania , Afrika na Dunia kwa ujumla. Baadhi ya mambo hayo ni:


1. UJINGA 




Mwalimu Nyerere alikuwa ni miongoni mwa wasomi wachache na ni mtanzania wa kwanza kupata nafasi yamasomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Edinburg , Uingereza na kuhitimu mwaka 1952 akiwa ni gwiji wa uchumi na historia.

Mwalimu hakupenda ujinga na hivyo alipigana vita kali dhidi ya ujinga, na alifanikiwa kwa nafasi yake kuwaondoa ujinga watanzania wengi, Ndiyo maana Rais Kikwete Februari 3, 2007 alisema “….sisi tuliwekezwa na ni lazima tuwekeze kwenu ili miaka 30 ijayo Rais atoke miongoni mwenu….”






2. UBINAFSI NA UFISADI 

Katika mambo aliyoyaamini sana na kuyapa mkazo wa aina yake, ni pamoja na masuala ya haki na usawa. Mwalimu siku zote, alijenga imani katika misngi ya utu, haki na usawa kwa kila raia wa dunia hii. Aidha Mwalimu alipinga sana mianya ya unyonyaji aliyoiita ‘mirija’. Mwalimu alipinga sera zozote zinazweza kuleta matabaka katika Taifa, iwe ni matabaka ya kiuchumi kwa kuwa na kundi la walionacho na wasionacho. 
Mwalimu hakuruhusu ubinafsi na ufisadi ambao ambao leo hii umekithiri miongoni mwa viongozi wengi hapa nchini. 
Mwalimu aliwahi kusema “Hakuna mtu yeyote katika jamii atakayekuwa na mahitaji yote muhimu wakati wengine katika jamii hiyohiyo hawana chochote”. 
Mwalimu alijikita katika siasa ya ‘ujamaa’ na kujitegemea na hatimaye Azimio la Arusha mwaka 1967, ili kahakisha keki ya Taifa [National cake] inakuwa na mgawanyo sawa kwa wote.
Mwaka 1978 nchi yetu ilikuwa katika wakati mgumu wa vita dhidi ya Nduli Iddiamin Dada, lakini wabunge walihitaji nyongeza ya mishahara na kupunguzwa posho ya waanafunzi wa elimu ya juu. Hali hii ilipelekea wanafunzi wa enzi hiyo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kugoma na kupinga ubinafsi wa waung hao. Hapa tuliona msimamo, uzalendo na busara za Mwalimu aliyetoa kauli kali ya kuamuru mishahara ya wabunge ipunguzwe na posho za vijana zibaki kama awali.
3. UBEPARI 
Mwalimu alikuwa ni nuru ing’aayo gizani, alipinga mfumo wa ubepari kwa kuuita ‘mfumo wa ufukarishaji’. Hivyo aliimarisha misingi imara katika itikadi yake ya ujamaa na kujitegemea, ikiwa ndiyo itikadi pekee yenye misingi ya utu, haki na usawa. 
Mwalimu alichukizwa sana na mfumo mpya wa kibepari uliozuka baada ya yeye kung’atuka madarakani aliouita ‘ubepari wa pembezoni’ yaani ni ubepari wa kishenzi unaotoa mianya kwa wachache kutumia mirija kuwanyonya wanyonge. 
Katika kitabu chake Ungozi wetu na hatima ya Tanzania ukurasa wa 28 Mwalimu alisema “Halimashauri kuu ya Taifa iliketi unguja, ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi, na walikuwa na haki ya kufanya hivyo maana sera ni yao.Ubaya wao ni kwamba, jambo lenyewe walilifanya kwa hila na janjajanja na mpaka sasa wanaendelea kuwadanganya wananchi kwamba sera ya CCM ni ya ujamaa na Kujitegemea.”
4. UKABILA NA USEHEMU 
Wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam , alifanikiwa kuwaunganisha wanafunzi katika jumuiya moja iitwayo USARF ikijumuisha wanafunzi kutoka nchi zote za Afrika. Aliona kuwa ni vema kwani Afrrika ni moja. Leo hii wanafunzi wetu wanajitambulisha na kujitanabaisha kwa makabila na sehemu watokazo. 
USARF imekufa kabisa na imebezwa na vijikundi vya makabila yao .
5. UBINAFSISHAJI HOLELA WA MALI ZA UMMA 
Wakati wa uhai wake Mwalimu alilaani vikali ubinafsishaji holela wa masirika ya umma. Alwakataa Mabeberu waliojiita ‘wawekezaji’ walionuiya kufirisi utajiri wa nchi yetu huku wakishibisha matumbo yao . 

6. KUONGOZWA KWA RIMOTI NA NCHI MATAJIRI 
Nakumbuka siku moja Mwalimu Nyerere akiwa katika viwanja vya mnazi mmoja [Dar es salaam] aliwahi kusema “Tangu lini IMF ikawa International Ministry of Finance?” [Wizara ya fedha ya kimataifa]. 
Leo hii viwanja hivyohivyo vinatumika kuusifu ubeberu wa IMF na wawekezaji wake, huku tukiwekewa masharti magumu ya kuongoza nchi yetu kwa maslahi ya mabeberu.
Mwalimu aliwaonya mataifa tajiri wasiingilie mambo yetu ya ndani, pale walipoona maslahi yao hayazingatiwi, mara kwa mara walimuhoji Mwalimu ambapo yeye aliwaamuru waondoke haraka na misaada yao yote. 
Mwalimu hakupenda misaada ya kinafiki iliyolenga kuwaangamiza wananchi wake, alipinga amri na maagizo ya taasisi za fedha kama Benki ya Dunia [WB] na IMF [International Monetary Fund].Hivyo aliheshimu maamuzi yake sahihi katika kulinda heshima ya nchi yetu na watu wake.
Kipindi chote cha uhai wake Mwalimu alisisitiza haja ya mataifa ya Afrika kujitawala na kuwa huru katika kujiamulia mambo yake. “Inapotokea taifa kuuza uhuru wake kwa ajili ya misaada ya kiuchumi au kukubali kukaliwa na majeshi ya nje, taifa hilo linakuwa limepotea na litanyonywa na watu wake watakuwa wanakandimizwa popote pale” alisema Mwalimu.
7. UBABE NA VITISHO KATIKA UONGOZI
Mwalimu aliamini kuwa kiongozi bora hapaswi kuwa na jazba na asiyetumia ubabe wala vitisho katika maamuzi au katika kutatua tatizo ambalo jamii inataka litatuliwe kwa maslahi na manufaa ya Taifa. Aliamini kuwa kiongozi bora ni yule anayeruhusu mianya ya majadiliano baina yake na wale anaowaongoza. Asiyetumia lugha chafu au kashfa na kejeli kwa watu wake.
8. UMANGIMEZA NA UKIRITIMBA
Wakati wa uhai wake Mwalimu aliheshimu mipaka, taasisi za utawala na mali za umma. Alichukia matumizi mabaya ya rasilimali za umma, pia aliheshimu mawazo yake mwenyewe na ya wenzake.
Mwalimu aliamini kwamba, kiongozi asiyepeda ukiritimba na umangimeza ni lazima awe mfuasi mzuri wa maadili anayoyasimamia, mwaminifu na mwadilifu kwa manufaa ya Taifa lake. Mwalimu hakupenda kutetea uovu wa viogozi eti kwa kutunza heshima zao au kulinda vyama vyao bila kujali uhusiano wao wala majina yao . Hivyo katika serikali yake Mwalimu hakuawa na ubia na mtu yeyote duniani.

9. USIRI WA MIKATABA NA MAKAMPUNI YA KIGENI 
Mwalimu alisisitiza uwazi katika mikataba mbalimbali ambayo serikali iliingia na makampuni ya kigeni.
Katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo Mwalimu anasema “Viongozi wa kiserikali wana wajibu mkubwa wa kuwafahamisha wananchi nini serikali inafanya na kwa sababu gain”
Tofauti kabisa hali ilivyo sasa, hali inayopelekea minung’uniko na malumbano yanayo husisha hata ugawaji wa tenda za serikali. Labda tuangalie mfano mmoja tu wa Mkataba wa Buzwagi ambao ulikuwa ni maarufu kama ‘Mkataba wa Karamagi’ kati ya Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi na Kampuni ya Barrik Gold Mine. Mkataba huu ulikuwa ni siri kubwa baina ya Barrik na Waziri tu, hali iliyopelekea Mbunge Zitto Kabwe kusimamishwa shughuli za bunge kwa miezi minne baada ya yeye kuhoji uhalali na uharaka wa utiaji saini mkataba huo uliosainiwa hotelini [Churchil Hotel] mjini London Uingereza.
10. RUSHWA 
Katiba ya CCM katika ahadi yake ya nne [4] ina sema “rushwa ni adui wa haki, sitatoa rushwa wala kupokea rushwa”. Jambo la rushwa pia Mzee wetu mpendwa Mwl Nyerere alilikemea vikali enzi za uhai wake kwani alijua wazi kuwa rushwa ni kikwazo cha maendeleo ya umma katika kila Taifa.
Nakumbuka Mh Kabuye [Mb-TLP] aliwahi kuwashutumu bungeni kuwa anauhakika wabunge wote waliingia kwa rushwa, wabunge hao walioshutumiwa walimtaka Kabuye afute kauli naye alisema “ kwa kulazimishwa nafuta kauli”. Walimlazimisha lakini hoja yake ilibaki kuwa ni ya msingi.
11. UCHU WA MADARAKA 
Mwl Nyerere ni miongoni mwa viongozi wachache sana duniani waliokosa kuwa na uchu wa madaraka. Ni miaka 24 sasa tangu Mwl ang’atuke madarakani kwa hiari yake akiwa kama rais wa awamu ya kwanza wa nchi yetu na ni miaka 22 tangu aachie uongozi wa CCM kama Mwenyekiti wa chama. Ndipo alipoamua kwa hiari yake kurejea Butihama na kuendeleza kilimo. 
Chanzo: Jambotz8

No comments

SIRI ZA JAMII. Powered by Blogger.