SINGAPORE KUMNYONGA RAIA WA NIGERIA KWA KUKUTWA NA MZIGO WA BANGI
Singapore imekataa ombi la msamaha
kutoka kwa raia mmoja wa Nigeria ambaye amepangiwa kunyongwa Ijumaa kwa
kupatikana na bangi, shirika la haki za kibinadamu la Amnesty
International limesema.
Familia ya Chijoke Stephen Obioha ilifahamishwa kuhusu hatua hiyo Jumatano.
Obioha alipatikana na kilo 2.6 za bangi Aprili 2007, kiasi
kilichokuwa kimezidi kipimo cha gramu 500 ambacho mara moja humfanya mtu
kuhukumiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya chini ya sheria za
Singapore.
Afisa wa Amnesty International Rafendi Djamin amesema
shirika hilo limeshangazwa na hatua hiyo ya Singapore kumnyima mshtakiwa
huyo msamaha.
Hata hivyo, alisema shirika hilo bado lina
matumaini kwamba Singapore haitatekeleza adhabu hiyo "katili na
isiyoweza kubatilishwa dhidi ya mtu huyo aliyehukumiwa kifo kwa kosa
ambalo halifai adhabu ya kifo."
"Hukumu ya kifo si suluhu.
Haitaangamiza dawa zote za kulevya Singapore. Kwa kuwanyonga watu kwa
makosa ya kuwa na dawa za kulevya, ambayo hayafikii kiwango cha makosa
makubwa ya uhalifu, Singapore inakiuka sheria za kimataifa.
"Mataifa mengi ulimwenguni yameacha adhabu hii ya kikatili, kinyama na ya kuhuzunisha."
Leave a Comment