MWENYEKITI WA VYAMA VYA SIASA SHIBUDA: NITAIMARISHA UHUSIANO KATI YA UKAWA NA CCM
Mwenyekiti mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda
ametamba kuwa ataimarisha uhusiano wa kisiasa kati ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) na Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.
Shibuda ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Ada Tadea, alitoa tambo hizo
jana, ikiwa ni dakika chache baada ya kuchaguliwa kuongoza baraza hilo
kwa kipindi cha miaka miwili katika uchaguzi uliofanyika jijini Dar
akichukua nafasi ya Peter Kuga Mziray wa APPTMaendeleo kilichofutwa na
Msajili wa Vyama vya Siasa.
Shibuda alisema atatumia fursa, uzoefu na uwezo alionao kuhakikisha
vyama vyote vinakuwa na matumaini ya ushiriki wa kisiasa kupitia heshima
ya baraza hilo.
“Nimepokea kwa furaha matokeo haya lakini najua nina mzigo mbele yangu.
Hilo la mahusiano ninamtanguliza Mungu anisaidie ili kuhakikisha
naotesha matumaini mapya katika baraza hili. Nitakunjua vizibo vyote
vilivyoziba katika mahusiano haya, ushirikiano wa siasa zetu uwe kwa
masilahi ya Watanzania na utaifa wetu,” alisema mbunge huyo wa zamani wa
CCM na Chadema.
Shibuda aliibuka mshindi baada ya kupata kura 20 dhidi ya mpinzani wake,
Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda aliyefuata kwa kura 14.
Jumla ya kura 36 zilipigwa huku mbili zikiharibika. Katibu wa CCK,
Renatus Muabhi alipongeza ushindi wa Shibuda huku akitoa angalizo kuwa
asikubali kutumika kulinda masilahi ya kundi la chama kilichopo
madarakani.
“Namwamini kwa uzoefu wake atasaidia kurejesha heshima ya baraza hilo
ila kama atayumbishwa, sisi tuko tayari kushawishi kura ya kumwondoa
madarakani,” alisema.
Wengine waliogombea kiti hicho ni Hashim Rungwe (Chaumma), Anna Mghwira
(ACT), Fahmy Dovutwa (UPDP), Hassan Kisavya (NRA), na John Cheyo wa UDP
ambaye alijitoa.
Baadhi ya vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi huo ni Sauti ya Umma
(Sau), CUF, CCM, DP, Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, Ada-Tadea, CCK na
Chadema.
Baraza la Vyama vya Siasa ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya
Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka jukwaa la kujadiliana masuala yenye
masilahi kwa Taifa na uimarishaji wa mfumo wa vyama vingi nchini.
Leave a Comment