SHERIA: WAJIBU WA MSIMAMIZI WA MIRATHI NA MAOMBI YA KUPEWA USIMAMIZI WA MUDA WA MIRATHI



Maombi ya Kupewa Usimamizi wa Muda wa Mirathi
Wakati maombi ya kuomba usimamizi au utekelezaji wa mirathi yanaendelea mahakamani, mwombaji anaweza kuiomba mahakama impe usimamizi wa mirathi wa muda. Msimamizi aliyepewa usimamizi wa muda anakuwa na majukumu sawa na msimamizi aliyethibitishwa au kuteuliwa na mahakama ya kukusanya na kutunza mali ya marehemu, isipokuwa hawezi kugawa mali ya marehemu kwa warithi. Lengo la kutoa usimamizi huu wa muda, ni kuwawezesha kutimiza majukumu ya haraka kama vile matunzo kwa watoto na mjane.


Wajibu wa Mtekelezaji au Msimamizi wa Mirathi Kadiri ya Jedwali la tano la Sheria ya Mahakama za Mahakimu na fungu la 99 la Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa mali
za marehemu, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi ya marehemu ndiye mwakilishi wa marehemu kisheria na mali zote za marehemu ziko mikononi mwake. Hivyo mtekelezaji au msimamizi wa mirathi ya marehemu anao wajibu na au majukumu kama inavyoainishwa hapa chini;


• Kukusanya mali zote za marehemu kwa uaminifu na
uangalifu mkubwa,


• Kupeleka orodha ya mali ya marehemu au madeni
alivyoweza kukusanya,


• Kupokea na kulipa madeni halali ya marehemu, ikiwani
pamoja na kulipa gharama zitokanazo na usimamizi,


• Kugawanya mali iliyobaki kwa warithi halali wa marehemu,


• Kuifahamisha mahakama juu ya ugawaji wa mali za
marehemu ulivyofanyika na kama umekamilika au muda
zaidi uongezwe ili aweze kukamilisha ugawaji wa mali ya
marehemu na kuiwezesha mahakama kufunga jalada la
mirathi,


• Kulingana na fungu la 100 la Sheria ya Mirathi na Usimamizi
wa Mali za Marehemu, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi
anaweza kushitaki au kushitakiwa katika shauri lolote jipya
au ambalo marehemu ama alianzisha au lilifunguliwa dhidi
yake,


• Kadri atakavyoona inafaa, na kadiri ilivyo kwa masilahi
ya warithi, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi, anaweza
kuuza mali inayohamishika kutoka katika mirathi ya
marehemu,


• Mtekelezaji au msimamizi wa mirathi hawezi kutengeneza
au kupata faida kutokana na usimamizi wake,isipokuwa
kama wosia umesema hivyo.


Angalizo Muhimu: Msimamizi wa mirathi yeye siyo mrithi wa
mali ya marehemu. Maana kumekuwepo na dhana potofu kwa
watekelezaji au wasimamizi wa mirathi walio wengi, kwamba
baada ya mtu kuthibitishwa au kuteuliwa kuwa mtekelezaji au
msimamizi wa mirathi, basi amerithishwa mali hizo moja kwa
moja na anaweza akafanya anavyotaka juu ya mali hizo. Kisheria
jambo hilo si la kweli na hiyo ni dhana potofu. Baada ya kuteuliwa
au kuchaguliwa kuwa msimmizi wa mirathi, anao wajibu wa
kukusanya mali na kuzigawa kwa warithi halali wa marehemu,
katika muda uliopangwa na kutoa taarifa mahakamani kwamba
zoezi hilo limefanyika salama na limekamilika. Kinyume na
hapo, anatenda kosa la jinai.

No comments

SIRI ZA JAMII. Powered by Blogger.